23 Nayo nchi haitauzwa kabisa kabisa; kwani nchi ni yangu mimi; maana ninyi ni wageni na wasafiri wangu.
24 Nanyi mtatoa ukombozi kwa ajili ya nchi, katika nchi yote ya milki yenu.
25 Kwamba nduguyo amekuwa maskini, na kuuza sehemu ya milki yake, ndipo jamaa yake aliye karibu naye atakuja, naye ataikomboa ile aliyoiuza nduguye.
26 Na kama mtu hana atakayeikomboa, naye mwenyewe amepata mali na kujiona kuwa anayo ya kutosha kuikomboa;
27 ndipo na aihesabu hiyo miaka ya kuuzwa kwake, na kilichozidi kumrudishia huyo mtu aliyeinunua; naye atairejea milki yake.
28 Lakini asipoweza kujipatia mwenyewe, ndipo hiyo iliyouzwa itakaa mkononi mwake huyo aliyeinunua, hata mwaka wa yubile; na katika yubile itatoka, naye atairejea milki yake.
29 Tena kwamba mtu anauza nyumba ya kukaa, iliyo ndani ya mji wenye kuta, ndipo ana ruhusa kuikomboa katika mwaka mmoja mzima baada ya kuiuza; atakuwa na amri ya kuikomboa muda wa mwaka mzima.