4 ndipo itakapokuwa, akiwa amefanya dhambi, na kupata hatia, atarudisha hicho alichokipata kwa kunyang’anya, au kitu kile alichokipata kwa kuonea, au ile amana aliyowekewa, au kitu kile kilichopotea alichokizumbua yeye,
5 au kitu cho chote ambacho amekiapia uongo; atakirudisha hata kwa utimilifu wake, kisha ataongeza na sehemu ya tano zaidi juu yake; naye atampa huyo mwenyewe, siku hiyo ambayo atakapohukumiwa kuwa mwenye hatia.
6 Kisha ataleta sadaka yake ya hatia kwa BWANA, ni kondoo mume wa katika kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, na kumpa kuhani;
7 na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA, naye atasamehewa; katika jambo lo lote alifanyalo hata akapata kuwa mwenye hatia kwalo.
8 BWANA akanena na Musa na kumwambia,
9 Haya, mwagize Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya sadaka ya kuteketezwa ni hii; hiyo sadaka ya kuteketezwa itakuwa pale motoni juu ya madhabahu usiku wote hata asubuhi; na huo moto wa madhabahu utawaka juu yake usizimike.
10 Naye kuhani atavaa nguo yake ya kitani, na suruali zake za kitani atazivaa mwilini mwake; naye atayazoa majivu ambayo huo moto umeiteketezea sadaka juu ya madhabahu, kisha atayaweka kando ya madhabahu.