5 au kitu cho chote ambacho amekiapia uongo; atakirudisha hata kwa utimilifu wake, kisha ataongeza na sehemu ya tano zaidi juu yake; naye atampa huyo mwenyewe, siku hiyo ambayo atakapohukumiwa kuwa mwenye hatia.
6 Kisha ataleta sadaka yake ya hatia kwa BWANA, ni kondoo mume wa katika kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, na kumpa kuhani;
7 na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA, naye atasamehewa; katika jambo lo lote alifanyalo hata akapata kuwa mwenye hatia kwalo.
8 BWANA akanena na Musa na kumwambia,
9 Haya, mwagize Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya sadaka ya kuteketezwa ni hii; hiyo sadaka ya kuteketezwa itakuwa pale motoni juu ya madhabahu usiku wote hata asubuhi; na huo moto wa madhabahu utawaka juu yake usizimike.
10 Naye kuhani atavaa nguo yake ya kitani, na suruali zake za kitani atazivaa mwilini mwake; naye atayazoa majivu ambayo huo moto umeiteketezea sadaka juu ya madhabahu, kisha atayaweka kando ya madhabahu.
11 Kisha atayavua mavazi yake, na kuvaa mavazi mengine, kisha atayachukua yale majivu kwenda nayo nje ya marago hata mahali safi.