30 Kisha Musa akatwaa baadhi ya mafuta ya kutia, na ya damu iliyokuwa pale juu ya madhabahu, na kumnyunyizia Haruni, katika mavazi yake, na wanawe, katika mavazi yao, pamoja naye; akamtakasa Haruni, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye.
31 Kisha Musa akawaambia huyo Haruni na wanawe, Tokoseni hiyo nyama mlangoni pa hema ya kukutania; mkaile pale pale, na hiyo mikate iliyo katika kile kikapu cha kuwaweka wakfu, kama nilivyoagizwa kusema, Haruni na wanawe wataila.
32 Nacho kitakachosalia katika hiyo nyama na mikate mtakichoma moto.
33 Wala msitoke nje mlangoni pa hema ya kukutania muda wa siku saba, hata siku za kuwekwa wakfu kwenu zitakapotimia; kwa kuwa atawaweka muda wa siku saba.
34 Vile vile kama vilivyotendeka siku ya leo, ni vivyo BWANA alivyoagiza kufanywa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
35 Nanyi mtakaa mlangoni pa hema ya kukutania muda wa siku saba mchana na usiku, na kuulinda ulinzi wa BWANA ili kwamba msife; kwani ndivyo nilivyoagizwa.
36 Basi Haruni na wanawe wakafanya mambo hayo yote BWANA aliyoyaagiza kwa mkono wa Musa.