1 Sasa utajikusanya vikosi vikosi, Ee binti wa vikosi; yeye amemhusuru; watampiga mwamuzi wa Israeli shavuni mwake kwa fimbo.
2 Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.
3 Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli.
4 Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za BWANA, kwa enzi ya jina la BWANA, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia.
5 Na mtu huyu atakuwa amani yetu; wakati Mwashuri atakapoingia katika nchi yetu, na kuyakanyaga majumba yetu, hapo mtaondokesha wachungaji saba juu yake, na wakuu wanane.
6 Nao wataiharibu nchi ya Ashuru kwa upanga, na nchi ya Nimrodi katika malango yake; naye atatuokoa na Mwashuri, atakapoingia katika nchi yetu, na kukanyaga ndani ya mipaka yetu.