5 BWANA akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu.
6 BWANA akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya.
7 Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao.
8 Basi BWANA akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji.
9 Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo BWANA alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko BWANA akawatawanya waende usoni pa nchi yote.
10 Hivi ndivyo vizazi vya Shemu; Shemu alikuwa mtu wa miaka mia akamzaa Arfaksadi miaka miwili baada ya gharika.
11 Shemu akaishi baada ya kumzaa Arfaksadi miaka mia tano, akazaa wana, waume na wake.