10 Neno hili alilolifanya likawa baya machoni pa BWANA, basi akamwua yeye naye.
11 Yuda akamwambia Tamari mkwewe, Ukae mjane nyumbani mwa baba yako hata Shela mwanangu atakapokuwa mtu mzima, maana alisema, Asipate kufa yeye kama nduguze. Basi Tamari akaenda, akakaa nyumbani mwa babaye.
12 Siku nyingi zikapita, akafa binti Shua, mkewe Yuda. Yuda akafarijika, akaenda kwa watu wake wawakatao manyoya kondoo huko Timna, yeye na mwenzake Hira, Mwadulami.
13 Huyo Tamari akapewa habari, kusema, Mkweo anakwenda Timna, akate manyoya ya kondoo zake.
14 Basi akavua nguo za ujane wake, akajivika utaji, akajifunika uso, akakaa mlangoni pa Enaimu, karibu na njia ya kuendea Timna. Maana aliona ya kwamba Shela amekuwa mtu mzima, wala hakuozwa awe mkewe.
15 Yuda alipomwona alimdhania kuwa ni kahaba, maana amejifunika uso.
16 Akamgeukia kando ya njia, akasema, Niruhusu niingie kwako. Maana hakujua ya kuwa ni mkwewe. Akamwuliza, Utanipa nini, ukiingia kwangu?