21 Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani.
22 Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili.
23 Na babaye akampelekea kama hivi, punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula kwa babaye njiani.
24 Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani.
25 Wakatoka Misri, wakafika nchi ya Kanaani kwa Yakobo, baba yao.
26 Wakampasha habari, wakisema, Yusufu angali hai; naye ndiye mtawala katika nchi yote ya Misri. Moyo wake ukazimia, kwa sababu hakuwasadiki.
27 Wakamwambia maneno yote ya Yusufu, aliyowaambia; na alipoona magari aliyoyapeleka Yusufu, ili kumchukua, roho ya Yakobo baba yao ikafufuka.