17 Wakaleta wanyama wao kwa Yusufu; Yusufu akawapa chakula badala ya farasi, na badala ya kondoo, na badala ya ng’ombe, na badala ya punda, naye akawalisha chakula badala ya wanyama wao wote mwaka ule.
18 Na mwaka ule ulipokwisha wakamjia mwaka wa pili, wakamwambia, Hatumfichi bwana wetu ya kwamba fedha zetu zimekwisha, na makundi ya wanyama ni mali ya bwana wetu, hakikusalia kitu mbele ya bwana wetu, ila miili yetu na nchi zetu.
19 Kwa nini tufe mbele ya macho yako, sisi na nchi yetu? Utununue sisi na nchi yetu kwa chakula, na sisi na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao; kisha utupe mbegu, tuishi wala tusife, wala nchi yetu isipotee.
20 Basi Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri; maana Wamisri waliuza kila mtu shamba lake; kwa sababu njaa ilikuwa imewazidi sana, nchi ikawa mali yake Farao.
21 Akawahamisha hao watu, akawaweka katika miji, tangu upande huu wa Misri hata upande huu.
22 Ila nchi ya makuhani hakuinunua; maana makuhani walikuwa na posho yao kutoka kwa Farao, wakala posho yao waliyopewa na Farao. Kwa hiyo hawakuuza nchi yao.
23 Yusufu akawaambia watu, Angalieni, nimewanunua leo, ninyi, na nchi yenu, kuwa mali ya Farao; basi mbegu zenu ni hizi, zipandeni katika nchi.