11 Dunia ikaharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma.
12 Mungu akaiona dunia, na tazama, imeharibika; maana kila mwenye mwili amejiharibia njia yake duniani.
13 Mungu akamwambia Nuhu, Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia.
14 Ujifanyie safina ya mti wa mvinje; fanya na vyumba ndani ya safina, ukaifunike ndani na nje kwa lami.
15 Hivi ndivyo utakavyoifanya; mikono mia tatu urefu wa safina, mikono hamsini upana wake, na mikono thelathini kwenda juu kwake.
16 Uifanyie safina mwangaza, ukaumalize juu kiasi cha mkono mmoja; ukautie mlango wa safina katika ubavu wake; ukaifanyie dari tatu, ya chini, ya pili, na ya tatu.
17 Na tazama, nitaleta gharika ya maji juu ya nchi, niharibu kila kitu chenye mwili na pumzi ya uhai, kisiwepo chini ya mbingu; kila kilichoko duniani kitakufa.