1 Ikawa katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. Nami mpaka sasa sikuwa na huzuni mbele ya mfalme wakati wo wote.
2 Basi mfalme akaniambia, Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana.
3 Nikamwambia mfalme, Mfalme na aishi milele; kwani uso wangu usiwe na huzuni, iwapo mji, ulio mahali pa makaburi ya baba zangu, unakaa ukiwa, na malango yake yameteketezwa kwa moto?
4 Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba? Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni.
5 Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unipeleke mpaka Yuda, niuendee mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga.
6 Mfalme akaniuliza, (malkia naye ameketi karibu naye), Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Nawe utarudi lini? Hivyo mfalme akaona vema kunipeleka; nami nikampa muda.
7 Tena nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na nipewe nyaraka kwa maliwali walio ng’ambo ya Mto, ili waniache kupita mpaka nifike Yuda;