5 ili nipate kukitimiza kiapo nilichowaapia baba zenu, kuwapa nchi ijaayo maziwa na asali, kama ilivyo leo hivi. Ndipo nikajibu, nikasema, Amina, Ee BWANA.
6 Naye BWANA akaniambia, Hubiri maneno haya yote katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, ukisema, Yasikieni maneno ya maagano haya, mkayafanye.
7 Kwa maana naliwashuhudia sana baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, hata leo, nikiamka mapema na kuwashuhudia, nikisema, Itiini sauti yangu.
8 Lakini hawakutii, wala kutega masikio yao, bali walikwenda kila mtu katika ushupavu wa moyo wake mbaya; kwa hiyo nimeleta juu yao maneno yote ya maagano haya, niliyowaamuru wayafanye; lakini hawakuyafanya.
9 Naye BWANA akaniambia, Fitina imeonekana katika watu wa Yuda, na katika wenyeji wa Yerusalemu.
10 Wameyarudia maovu ya baba zao, waliokataa kusikia maneno yangu; wamewafuata miungu mingine na kuwatumikia; nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, wameyavunja maagano yangu niliyoyafanya na baba zao.
11 Basi, BWANA asema hivi, Tazama, nitaleta mabaya juu yao, ambayo hawataweza kuyakimbia; nao watanililia, walakini sitawasikiliza.