1 Neno la BWANA lililomjia Yeremia, katika habari ya ukosefu wa mvua.
2 Yuda huomboleza,Na malango yake yamelegea;Wameketi chini wamevaa kaniki;Na kilio cha Yerusalemu kimepaa juu.
3 Na wakuu wao huwatuma watoto wao kwenye maji;Nao hufika visimani wasione maji;Hurudi, na vyombo vyao ni vitupu;Wametahayarika na kufadhaika,Na kuvifunika vichwa vyao.
4 Kwa sababu ya nchi iliyopasuka,Kwa kuwa mvua haikunyesha katika nchi,Wenye kulima wametahayarika,Na kuvifunika vichwa vyao.
5 Naam, kulungu naye uwandani amezaa,Akamwacha mwanawe kwa kuwa hapana majani.
6 Na punda-mwitu husimama juu ya vilele vya milima,Hutwetea pumzi kama mbwa-mwitu;Macho yao hayaoni sawasawa,Kwa kuwa hapana majani.
7 Ijapokuwa maovu yetu yanatushuhudia, lakini utende wewe kwa ajili ya jina lako, Ee BWANA, maana kurudi nyuma kwetu ni kwingi; tumekutenda dhambi.