1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, hapo mfalme Sedekia alipompelekea Pashuri, mwana wa Malkiya, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, kusema,
2 Tafadhali utuulizie habari kwa BWANA; kwa maana Nebukadreza, mfalme wa Babeli, analeta vita juu yetu; labda BWANA atatutendea sawasawa na kazi zake zote za ajabu, ili aende zake akatuache.
3 Basi Yeremia akawaambia, Mwambieni Sedekia neno hili,
4 BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Angalieni, nitazigeuza nyuma silaha za vita zilizo mikononi mwenu, ambazo kwa hizo ninyi mnapigana na mfalme wa Babeli, na Wakaldayo, wanaowahusuru nje ya kuta zenu, nami nitazikusanya pamoja katikati ya mji huu.
5 Na mimi mwenyewe nitapigana nanyi, kwa mkono ulionyoshwa na kwa mkono hodari, naam, kwa hasira, na kwa ukali, na kwa ghadhabu nyingi.