2 Tafadhali utuulizie habari kwa BWANA; kwa maana Nebukadreza, mfalme wa Babeli, analeta vita juu yetu; labda BWANA atatutendea sawasawa na kazi zake zote za ajabu, ili aende zake akatuache.
3 Basi Yeremia akawaambia, Mwambieni Sedekia neno hili,
4 BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Angalieni, nitazigeuza nyuma silaha za vita zilizo mikononi mwenu, ambazo kwa hizo ninyi mnapigana na mfalme wa Babeli, na Wakaldayo, wanaowahusuru nje ya kuta zenu, nami nitazikusanya pamoja katikati ya mji huu.
5 Na mimi mwenyewe nitapigana nanyi, kwa mkono ulionyoshwa na kwa mkono hodari, naam, kwa hasira, na kwa ukali, na kwa ghadhabu nyingi.
6 Nami nitawapiga wenyeji wa mji huu, wanadamu na wanyama pia; watakufa kwa tauni kubwa.
7 Na baada ya hayo, asema BWANA, nitamtia Sedekia, mfalme wa Yuda, na watumishi wake, na watu wote waliosalia ndani ya mji huu, baada ya tauni ile, na upanga, na njaa, katika mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na katika mikono ya adui zao, na katika mikono ya watu wale wanaowatafuta roho zao; naye atawaua kwa ukali wa upanga; hatawaachilia, wala hatawahurumia, wala hatawarehemu.
8 Nawe waambie watu hawa, BWANA asema hivi, Tazama naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti.