6 Nami nitawapiga wenyeji wa mji huu, wanadamu na wanyama pia; watakufa kwa tauni kubwa.
7 Na baada ya hayo, asema BWANA, nitamtia Sedekia, mfalme wa Yuda, na watumishi wake, na watu wote waliosalia ndani ya mji huu, baada ya tauni ile, na upanga, na njaa, katika mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na katika mikono ya adui zao, na katika mikono ya watu wale wanaowatafuta roho zao; naye atawaua kwa ukali wa upanga; hatawaachilia, wala hatawahurumia, wala hatawarehemu.
8 Nawe waambie watu hawa, BWANA asema hivi, Tazama naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti.
9 Yeye atakayekaa katika mji huu atakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; bali yeye atakayetoka, na kujitia pamoja na Wakaldayo wanaowahusuru, yeye ataishi, na maisha yake yatakuwa nyara kwake.
10 Maana nimeweka uso wangu juu ya mji huu niuletee mabaya, wala nisiuletee mema, asema BWANA; utatiwa katika mkono wa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza.
11 Na katika habari za nyumba ya mfalme wa Yuda, lisikieni neno la BWANA,
12 Ee nyumba ya Daudi, BWANA asema hivi, Hukumuni hukumu ya haki asubuhi, mkawaponye waliotekwa nyara na mkono wake aliyewadhulumu, ghadhabu yangu isije ikatoka kama moto, ikaunguza, asiweze mtu ye yote kuuzima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.