1 BWANA akasema hivi, Shuka nyumbani kwa mfalme wa Yuda, ukaseme neno hili huko,
2 ya kwamba, Sikia neno la BWANA, Ee mfalme wa Yuda; wewe uketiye katika kiti cha enzi cha Daudi, wewe, na watumishi wako, na watu wako wote waingiao kwa malango haya;
3 BWANA asema hivi, Fanyeni hukumu na haki, mkamtoe yeye aliyetekwa katika mikono ya mdhalimu; wala msiwatende mabaya mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kuwadhulumu, wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia katika mahali hapa.
4 Kwa maana mkifanya haya kweli kweli, ndipo watakapoingia kwa malango ya nyumba hii wafalme wenye kuketi katika kiti cha enzi cha Daudi, wanakwenda kwa magari, na wamepanda farasi yeye, na watumishi wake, na watu wake.