7 Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema BWANA, ambapo hawatasema tena, Aishivyo BWANA, aliyewatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri;
8 lakini, Aishivyo BWANA, aliyewapandisha na kuwaongoza wazao wa nyumba ya Israeli kutoka nchi ya kaskazini, na kutoka nchi zote nilikowafukuza; nao watakaa katika nchi yao wenyewe.
9 Katika habari za manabii.Moyo wangu ndani yangu umevunjika,Mifupa yangu yote inatikisika.Nimekuwa kama mtu aliye mlevi,Na kama mtu aliyeshindwa na divai;kwa ajili ya BWANA, na kwa ajili ya maneno yake matakatifu.
10 Maana nchi imejaa wazinzi; kwa sababu ya kuapa nchi inaomboleza; malisho ya nyikani yamekauka; mwenendo wao ni mbaya, na nguvu zao si za haki.
11 Maana nabii, na kuhani, wote wawili wanakufuru; naam, katika nyumba yangu nimeuona uovu wao, asema BWANA.
12 Kwa ajili ya hayo njia yao itakuwa kwao kama mahali pa kuteleza gizani; watatelemshwa na kuanguka hapo; kwa maana nitaleta uovu juu yao, naam, mwaka wa kujiliwa kwao, asema BWANA.
13 Nami nimeona upumbavu katika manabii wa Samaria; walitabiri kwa Baali, wakawakosesha watu wangu Israeli.