4 Nawe utawaambia, BWANA asema hivi, Kama hamtaki kunisikia, kwenda katika sheria yangu, niliyoiweka mbele yenu,
5 kuyasikiliza maneno ya watumishi wangu, manabii, ninaowatuma kwenu, naam, nikiondoka mapema na kuwatuma; lakini ninyi hamkuwasikiliza;
6 basi, nitafanya nyumba hii kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya kuwa laana kwa taifa zote za dunia.
7 Na makuhani, na manabii, na watu wote, wakamsikia Yeremia, hapo aliposema maneno haya katika nyumba ya BWANA.
8 Ikawa, Yeremia alipokuwa amekwisha kusema maneno yote BWANA aliyomwamuru kuwaambia watu wote, ndipo hao makuhani, na manabii, na watu wote, wakamkamata, wakisema, Bila shaka utakufa.
9 Kwa nini umetabiri kwa jina la BWANA, ukisema, Nyumba hii itakuwa kama Shilo, na mji huu utakuwa ukiwa, hautakaliwa na mtu? Watu wote wakamkusanyikia Yeremia katika nyumba ya BWANA.
10 Na wakuu wa Yuda waliposikia habari za mambo haya, wakatoka katika nyumba ya mfalme, wakapanda juu mpaka nyumbani kwa BWANA; wakaketi, hapo watu waingiapo katika lango jipya la nyumba ya BWANA.