7 Na makuhani, na manabii, na watu wote, wakamsikia Yeremia, hapo aliposema maneno haya katika nyumba ya BWANA.
8 Ikawa, Yeremia alipokuwa amekwisha kusema maneno yote BWANA aliyomwamuru kuwaambia watu wote, ndipo hao makuhani, na manabii, na watu wote, wakamkamata, wakisema, Bila shaka utakufa.
9 Kwa nini umetabiri kwa jina la BWANA, ukisema, Nyumba hii itakuwa kama Shilo, na mji huu utakuwa ukiwa, hautakaliwa na mtu? Watu wote wakamkusanyikia Yeremia katika nyumba ya BWANA.
10 Na wakuu wa Yuda waliposikia habari za mambo haya, wakatoka katika nyumba ya mfalme, wakapanda juu mpaka nyumbani kwa BWANA; wakaketi, hapo watu waingiapo katika lango jipya la nyumba ya BWANA.
11 Ndipo hapo makuhani, na manabii, wakawaambia wakuu na watu wote, wakisema, Mtu huyu amestahili kufa, kwa sababu ametabiri juu ya mji huu, kama mlivyosikia kwa masikio yenu.
12 Ndipo Yeremia akawaambia wakuu wote na watu wote, akisema, BWANA ndiye aliyenituma kutabiri juu ya nyumba hii, na juu ya mji huu, maneno hayo yote mliyoyasikia.
13 Basi sasa, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, mkaisikilize sauti ya BWANA, Mungu wenu; naye BWANA atayaghairi mabaya aliyoyanena juu yenu.