1 Ikawa, katika mwaka ule ule, mwanzo wa kutawala kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, mwaka wa nne, mwezi wa tano, Hanania, mwana wa Azuri, nabii, wa Gibeoni, akasema nami ndani ya nyumba ya BWANA, mbele ya makuhani na watu wote, akisema,
2 BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimeivunja nira ya mfalme wa Babeli.
3 Kabla haujatimia muda wa miaka miwili mizima, nitavirudisha mahali hapa vyombo vyote vya nyumba ya BWANA, ambavyo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, aliviondoa katika mahali hapa, akavichukua mpaka Babeli.
4 Nami nitamrudisha hapa Yekonia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, pamoja na mateka wote wa Yuda, waliokwenda Babeli, asema BWANA; maana nitaivunja nira ya mfalme wa Babeli.
5 Ndipo nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, mbele ya makuhani, na mbele ya watu wote waliosimama ndani ya nyumba ya BWANA,
6 naam, nabii Yeremia akasema, Amina, BWANA na atende hivi; BWANA ayatimize maneno yako uliyotabiri, kuvirudisha hapa vyombo vya nyumba ya BWANA na watu wote waliofungwa, toka Babeli, hata mahali hapa.