4 Na haya ndiyo maneno aliyosema BWANA, katika habari za Israeli, na katika habari za Yuda.
5 Maana BWANA asema hivi, Tumesikia sauti ya tetemeko, na ya hofu, wala si ya amani.
6 Ulizeni sasa, mkaone kwamba mwanamume aona utungu wa uzazi; mbona, basi, ninaona kila mtu anaweka mikono yake viunoni, kama mwanamke aliye na utungu, na nyuso zote zimegeuka rangi.
7 Ole! Maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo, maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa nayo.
8 Na itakuwa katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, nitaivunja nira yake itoke shingoni mwako, nami nitavipasua vifungo vyako; wala wageni hawatamtumikisha tena;
9 bali watamtumikia BWANA, Mungu wao, na Daudi, mfalme wao, nitakayemwinua kwa ajili yao.
10 Kwa sababu hiyo usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu, asema BWANA; wala usifadhaike, Ee Israeli; kwa maana, tazama, nitakuokoa toka mbali, na wazao wako toka nchi ya uhamisho wao; na Yakobo atarudi, naye atatulia na kustarehe, wala hapana mtu atakayemtia hofu.