9 Basi nikalinunua shamba lile lililoko Anathothi kwa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, nikampimia fedha yake, shekeli kumi na saba za fedha.
10 Nami nikaitia sahihi ile hati, na kuipiga muhuri, nikawaita mashahidi, nikampimia ile fedha katika mizani.
11 Nikaitwaa ile hati ya kununua, ile iliyopigwa muhuri kama ilivyo sheria na ada, na ile nayo iliyokuwa wazi;
12 na ile hati ya kununua nikampa Baruku, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, mbele ya uso wa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, na mbele ya mashahidi wale walioitia sahihi hati ya kununua, mbele ya Wayahudi wote walioketi katika uwanda wa walinzi.
13 Nami nikamwagiza Baruku mbele yao, nikisema,
14 BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Twaa hati hizi, hati hii ya kununua, hati hii iliyopigwa muhuri, na hii iliyo wazi pia, ukazitie katika chombo cha udongo, zipate kukaa siku nyingi.
15 Maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nyumba na mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii.