8 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, baada ya wakati ule mfalme Sedekia alipofanya agano na watu wote waliokuwa katika Yerusalemu, kuwatangazia habari ya uhuru;
9 ya kwamba kila mtu amweke huru mtumwa wake, na kila mtu amweke huru mjakazi wake, ikiwa yule mwanamume au yule mwanamke ni Mwebrania; mtu ye yote asiwatumikishe, yaani, asimtumikishe Myahudi, nduguye;
10 na wakuu wote, na watu wote, wakati, waliofanya agano hilo, ya kwamba kila mtu amweke huru mtumwa wake na mjakazi wake, mtu ye yote asiwatumikishe tena; wakatii, wakawaacha.
11 Lakini baadaye wakaghairi, wakawarudisha watumwa wale, na wajakazi wale, ambao wamewaacha huru, nao wakawatia utumwani wawe watumwa na wajakazi wao.
12 Basi, neno la BWANA likamjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema,
13 BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalifanya agano na baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa, nikisema,
14 Mwisho wa kila mwaka wa saba kila mtu na amweke huru ndugu yake aliye Mwebrania, aliyeuzwa kwako na kukutumikia miaka sita utamwacha atoke kwako huru, lakini baba zenu hawakunisikiliza, wala hawakutega masikio yao.