1 BWANA asema hivi, Angalia, nitaamsha juu ya Babeli, na juu yao wakaao Leb-kamai, upepo uharibuo.
2 Nami nitapeleka wageni mpaka Babeli, watakaompepea; nao wataifanya nchi yake kuwa tupu; kwa kuwa katika siku ya taabu watakuwa juu yake pande zote.
3 Juu yake apindaye upinde, mwenye upinde na apinde upinde wake, na juu yake ajiinuaye katika dirii yake; msiwaachilie vijana wake; liangamizeni jeshi lake lote.
4 Nao wataanguka, hali ya kuuawa, katika nchi ya Wakaldayo, hali ya kutumbuliwa katika njia kuu zake.
5 Kwa maana Israeli, wala Yuda, hakuachwa na Mungu wake, BWANA wa majeshi; ijapokuwa nchi yao imejaa hatia juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli.
6 Kimbieni kutoka kati ya Babeli, kila mtu na ajiokoe nafsi yake; msikatiliwe mbali katika uovu wake; maana ni wakati wa kisasi cha BWANA, atamlipa malipo.
7 Babeli umekuwa kikombe cha dhahabu mkononi mwa BWANA; kilicholevya dunia yote; mataifa wamekunywa mvinyo wake; kwa sababu hiyo mataifa wameingiwa na wazimu.