44 Nami nitafanya hukumu juu ya Beli katika Babeli, nami nitavitoa katika kinywa chake alivyovimeza; wala mataifa hawatamwendea tena; naam, ukuta wa Babeli utaanguka.
45 Enyi watu wangu; tokeni katikati yake, mkajiokoe nafsi zenu na hasira kali ya BWANA, kila mmoja wenu.
46 Wala isizimie mioyo yenu, wala msiiogope habari itakayosikiwa katika nchi; maana habari itakuja mwaka mmoja, na baadaye mwaka wa pili habari itakuja, na udhalimu katika nchi, mwenye kutawala akishindana na mwenye kutawala.
47 Basi angalia, siku zitakuja, ambazo katika siku hizo, nitafanya hukumu juu ya sanamu za Babeli, na nchi yake yote itatahayarika; na watu wake wote waliouawa wataanguka katikati yake.
48 Ndipo mbingu, na nchi, na vitu vyote vilivyomo, vitaimba kwa furaha juu ya Babeli; kwa maana watu waangamizao watamjilia kutoka kaskazini, asema BWANA.
49 Kama vile Babeli alivyowaangusha watu wa Israeli waliouawa, ndivyo watakavyoanguka katika Babeli watu wa nchi yake nzima waliouawa.
50 Ninyi mliojiepusha na upanga,Enendeni zenu, msisimame;Mkumbukeni BWANA tokea mbali,Na Yerusalemu ukatiwe mioyoni mwenu.