58 BWANA wa majeshi asema hivi, Kuta pana za Babeli zitabomolewa kabisa, na malango yake marefu yatateketezwa; nao watu watajitaabisha kwa ubatili, na mataifa kwa moto; nao watachoka.
59 Neno ambalo Yeremia, nabii, alimwamuru Seraya, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, alipokwenda Babeli pamoja na Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa kumiliki kwake. Basi Seraya alikuwa msimamizi mkuu wa nyumba ya mfalme.
60 Naye Yeremia akaandika katika kitabu habari ya mabaya yote yatakayoupata Babeli, maneno hayo yote yaliyoandikwa juu ya Babeli.
61 Naye Yeremia akamwambia Seraya, Utakapofika Babeli, basi angalia uyasome maneno haya yote,
62 ukaseme, Ee BWANA, umenena habari za mji huu kwamba utakatiliwa mbali, usikaliwe na awaye yote, wala wanadamu wala wanyama, lakini uwe ukiwa hata milele.
63 Tena itakuwa utakapokwisha kukisoma kitabu hicho, utakifungia jiwe, na kukitupa katika mto Frati;
64 nawe utasema, Hivyo ndivyo utakavyozama Babeli, wala hautazuka tena, kwa sababu ya mabaya yote nitakayoleta juu yake; nao watachoka. Maneno ya Yeremia yamefika hata hapa.