14 basi, nitaitenda nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, mnayoitumainia, na mahali hapa nilipowapa ninyi na baba zenu, kama nilivyopatenda Shilo.
15 Nami nitawatupa ninyi mbali na macho yangu, kama nilivyowatupa ndugu zenu wote, yaani, wazao wote wa Efraimu.
16 Basi, wewe usiwaombee watu hawa, wala usiwapazie sauti yako, wala kuwaombea dua, wala usinisihi kwa ajili yao; kwa maana sitakusikiliza.
17 Je! Huoni wanavyotenda katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu?
18 Watoto huokota kuni, na baba zao huwasha moto, na wanawake hukanda unga, ili kumfanyizia mikate malkia wa mbinguni, na kuwamiminia miungu mingine sadaka za kinywaji, wapate kunikasirisha mimi.
19 Je! Watu hawa wanikasirisha mimi? Asema BWANA; hawajikasirishi nafsi zao, na kuzitia haya nyuso zao wenyewe?
20 Kwa hiyo, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, hasira yangu na ghadhabu yangu zitamwagwa juu ya mahali hapa, juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya miti ya mashamba, na juu ya mazao ya nchi; nayo itateketea, isizimike.