1 Laiti kichwa changu kingekuwa maji, na macho yangu kuwa chemchemi ya machozi, ili nipate kulia mchana na usiku kwa ajili yao waliouawa wa binti ya watu wangu!
2 Laiti ningekuwa na mahali pa kukaa jangwani, kibanda cha wasafiri; nipate kuwaacha watu wangu, na kuondoka kwao! Maana wao ni wazinzi, wote pia, mkutano wa watu wenye hiana.
3 Huupinda ulimi wao, kana kwamba ni upinde, ili kusema uongo; nao wamepata nguvu katika nchi, lakini si katika uaminifu; maana huendelea toka ubaya hata ubaya, wala hawanijui mimi, asema BWANA.
4 Jihadharini, kila mtu na jirani yake, wala msimtumaini ndugu awaye yote; maana kila ndugu atachongea, na kila jirani atakwenda huko na huko na kusingizia.