Yos. 10:8-14 SUV

8 BWANA akamwambia Yoshua, Usiwache watu hao; kwa kuwa mimi nimekwisha kuwatia mikononi mwako; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesimama mbele yako.

9 Basi Yoshua akawafikilia ghafula; kwani alikwea kutoka Gilgali kwenda usiku kucha.

10 BWANA naye akawatapanya mbele ya Israeli, naye Israeli akawaua uuaji ulio mkuu hapo Gibeoni, akawafukuza waikimbilie hiyo njia ya kukwelea kwenda Beth-horoni, na kuwapiga hata kufikilia Azeka, tena hata kufikilia Makeda.

11 Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa katika kutelemkia Beth-horoni, ndipo BWANA alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hata kufikilia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga.

12 Ndipo Yoshua akanena na BWANA katika siku hiyo ambayo BWANA aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli,Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni;Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni.

13 Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia,Hata hilo taifa lilipokuwa limekwisha jipatiliza juu ya adui zao.Hayo, je! Hayakuandikwa ndani ya kitabu cha Yashari? Basi jua likasimama kimya katikati ya mbingu, wala halikufanya haraka kuchwa kama muda wa siku nzima.

14 Haikuwapo siku nyingine mfano wa siku hiyo katika siku zilizotangulia mbele yake wala katika hizo zilizoandama baada yake, hata ikawa yeye BWANA kuisikia sauti ya binadamu; kwa kuwa BWANA alipiga vita kwa ajili ya Israeli.