10 upande wa kusini ilikuwa ni mali ya Efraimu, na upande wa kaskazini ilikuwa ni mali ya Manase, na bahari ilikuwa mpaka wake; nao wakafikilia hata Asheri upande wa kaskazini, na kufikilia hata Isakari upande wa mashariki.
11 Tena Manase alikuwa na miji katika Isakari na katika Asheri, nayo ni hii, Bethsheani na vijiji vyake, na Ibleamu na miji yake, na wenyeji wa Dori na miji yake, na wenyeji wa Endori na miji yake, na wenyeji wa Taanaki na miji yake, na wenyeji wa Megido na miji yake, hata mahali patatu palipoinuka.
12 Lakini wana wa Manase hawakuweza kuwafukuza wenyeji wa miji hiyo; bali hao Wakanaani walijikaza ili wakae katika nchi hiyo.
13 Kisha ikawa, hapo hao wana wa Israeli walipokuwa wamepata nguvu zaidi, ndipo wakawatenza nguvu hao Wakanaani wafanye kazi ya shokoa, wala hawakuwafukuza kabisa.
14 Kisha wana wa Yusufu wakanena na Yoshua, wakasema, Kwa nini umenipa mimi kura moja tu na fungu moja kuwa ni urithi wangu, kwa kuwa mimi ni taifa kubwa la watu, kwa sababu BWANA amenibarikia hata hivi sasa?
15 Yoshua akawaambia, Kwamba wewe u taifa kubwa la watu, haya, kwea uende mwituni, ujikatie mahali hapo kwa ajili ya nafsi yako katika nchi ya Waperizi, na ya hao Warefai; ikiwa hiyo nchi ya vilima ya Efraimu ni nyembamba, haikutoshi.
16 Wana wa Yusufu wakasema, Hiyo nchi ya vilima haitutoshi sisi; lakini Wakanaani wote wakaao katika nchi ya bondeni wana magari ya chuma, hao walio katika Bethsheani na miji yake, na hao walio katika bonde la Yezreeli pia.