Yos. 18:8-14 SUV

8 Basi watu hao wakainuka wakaenda; kisha Yoshua aliwaagiza wale waliokwenda kuiandika nchi, akawaambia, Endeni, mkapite katikati ya nchi, na kuiandika habari zake, kisha mnijie tena hapa, nami nitawapigia kura kwa ajili yenu hapo mbele za BWANA huko Shilo.

9 Basi watu hao wakaenda, wakapita katikati ya nchi, wakaandika habari zake katika chuo, na kuigawanya kwa miji yake, hata iwe mafungu saba, kisha wakamrejea Yoshua maragoni huko Shilo.

10 Kisha Yoshua akapiga kura kwa ajili yao hapo mbele za BWANA katika Shilo; huko Yoshua akawagawanyia wana wa Israeli hiyo nchi sawasawa na mafungu yao.

11 Kisha ilizuka kura ya kabila ya wana wa Benyamini kwa kuandama jamaa zao; na mpaka wa hiyo kura yao ukatokea kati ya wana wa Yuda na wana wa Yusufu.

12 Mpaka wao upande wa kaskazini ulikuwa kutoka mto wa Yordani; kisha mpaka ukaendelea kufikilia ubavuni mwa mji wa Yeriko upande wa kaskazini, kisha ukaendelea kati ya nchi ya vilima kwa kuelekea upande wa magharibi; na matokeo yake yalikuwa hapo penye nyika ya Bethaveni.

13 Kisha mpaka ukaendelea kutoka hapo na kufikilia mji wa Luzu, ubavuni mwa Luzu (ndio Betheli), kwa upande wa kusini; kisha mpaka ukatelemkia Ataroth-adari, karibu na mlima ulio upande wa kusini wa Beth-horoni wa chini.

14 Kisha mpaka uliendelea na kuzunguka upande wa magharibi wa kuelekea kusini, kutoka huo mlima ulio mkabala wa Beth-horoni upande wa kusini; na matokeo yake yalikuwa hapo Kiriath-baali (ndio Kiriath-yearimu), ni mji wa wana wa Yuda; huo ndio upande wa magharibi.