Yos. 22:5-11 SUV

5 Lakini mjibidiishe sana kuzifanya amri na sheria, ambazo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwaamuru, kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kwenenda katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na kushikamana na yeye, na kumtumikia kwa moyo wenu wote na nafsi yenu yote.

6 Basi Yoshua akawabarikia, na kuwapa ruhusa waende zao; nao wakaenda mahemani kwao.

7 Basi Musa alikuwa amewapa hiyo nusu moja ya kabila ya Manase urithi katika Bashani; lakini hiyo nusu ya pili Yoshua aliwapa urithi kati ya ndugu zao, ng’ambo ya Yordani upande wa kuelekea magharibi. Zaidi ya hayo Yoshua, hapo alipowapeleka waende zao mahemani kwao, akawabarikia,

8 kisha akanena nao, na kuwaambia, Rudini na mali mengi mahemani kwenu, na ng’ombe wengi sana, na fedha, na dhahabu, na shaba, na chuma, na mavao mengi sana; mzigawanye na ndugu zenu hizo nyara za adui zenu.

9 Basi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase wakarudi, wakatoka kwa wana wa Israeli katika Shilo, ulioko nchi ya Kanaani, ili waende nchi ya Gileadi, hiyo nchi ya milki yao, waliyokuwa wanaimiliki, sawasawa na amri ya BWANA kwa mkono wa Musa.

10 Nao walipofika pande za Yordani, zilizo katika nchi ya Kanaani, hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na nusu ya kabila ya Manase, wakajenga madhabahu huko karibu na Yordani, iliyoonekana kuwa ni madhabahu kubwa.

11 Wana wa Israeli walisikia ikinenwa, Tazama, wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wamejenga madhabahu huko upande wa mbele wa nchi ya Kanaani, katika nchi iliyo karibu na Yordani, kwa upande huo ulio milki ya wana wa Israeli.