3 wakawaamuru watu wote wakisema, Mtakapoliona sanduku la agano la BWANA, Mungu wenu, na makuhani Walawi wakilichukua, ndipo mtakapoondoka hapa mlipo na kulifuata.
4 Lakini, na iwe nafasi kati ya ninyi na lile sanduku, kama dhiraa elfu mbili kiasi chake; msilikaribie mpate kuijua njia ambayo hamna budi kuiendea; kwa maana hamjapita njia hii bado.
5 Yoshua akawaambia watu, Jitakaseni; maana kesho BWANA atatenda mambo ya ajabu kati yenu.
6 Kisha Yoshua akawaambia makuhani, akasema, Liinueni sanduku la agano, mkavuke mbele ya hao watu. Wakaliinua sanduku la agano, wakatangulia mbele ya watu.
7 BWANA akamwambia Yoshua, Hivi leo nitaanza kukutukuza mbele ya Israeli wote, wapate kujua ya kuwa mimi nitakuwa pamoja na wewe, kama nilivyokuwa pamoja na Musa.
8 Nawe uwaamuru hao makuhani walichukuao sanduku la agano, ukawaambie, Mtakapofika ukingo wa maji ya Yordani, simameni katika Yordani.
9 Basi Yoshua akawaambia wana wa Israeli, Njoni huku, mkayasikie maneno ya BWANA, Mungu wenu.