2 Wakati huo BWANA akamwambia Yoshua, Haya, jifanyie visu vya mawe ya gumegume, watahiri tena wana wa Israeli mara ya pili.
3 Basi Yoshua akajifanyia visu vya mawe ya gumegume, akawatahiri wana wa Israeli huko Gibea-haaralothi.
4 Na sababu ya Yoshua kutahiri ni hii; watu wote waliotoka Misri, waliokuwa waume, hao watu waume wote waendao vitani walikufa katika bara njiani, baada ya wao kutoka Misri.
5 Kwa kuwa watu wote waliotoka walikuwa wamekwisha kutahiriwa; lakini watu wote waliozaliwa katika bara njiani walipokwisha kutoka Misri, hao hawakutahiriwa.
6 Kwa kuwa wana wa Israeli walitembea muda wa miaka arobaini barani, hata hilo taifa zima, yaani, watu waume waendao vitani, waliotoka Misri, walipokuwa wameangamia; kwa sababu hawakuisikiza sauti ya BWANA; nao ndio BWANA aliowaapia ya kwamba hatawaacha waione hiyo nchi, ambayo BWANA aliwaapia baba zao kwamba atatupa sisi; nchi ijaayo maziwa na asali.
7 Na watoto wao, aliowainua badala yao ndio hao aliowatahiri Yoshua; kwa kuwa wao walikuwa hawakutahiriwa, kwa maana walikuwa hawakuwatahiri njiani.
8 Ilikuwa walipokwisha kutahiriwa taifa zima, wakakaa kila mtu mahali pake maragoni, hata walipopoa.