6 Hao wanayo mamlaka ya kufunga anga, mvua isinyeshe wakati wanapotoa unabii. Tena wanayo mamlaka ya kuzigeuza chemchemi zote za maji ziwe damu, na ya kusababisha maafa ya kila namna duniani kila mara wanapopenda.
7 Lakini wakisha maliza kutoa unabii huo, mnyama atokaye shimoni kuzimu atapigana nao, atawashinda na kuwaua.
8 Maiti zao zitabaki katika barabara za mji mkuu ambapo Bwana wao alisulubiwa. Jina la kupanga la mji huo ni Sodoma au Misri.
9 Watu wa kila kabila, lugha, taifa na rangi wataziangalia maiti hizo kwa muda wa siku tatu na nusu, na hawataruhusu zizikwe.
10 Watu waishio duniani watafurahia kifo cha hao wawili. Watafanya sherehe na kupelekeana zawadi, maana manabii hawa wawili walikuwa wamewasumbua mno watu wa dunia.
11 Lakini baada ya zile siku tatu na nusu pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu iliwaingia, nao wakasimama; wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu.
12 Kisha, hao manabii wawili wakasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njoni hapa juu!” Nao wakapanda juu mbinguni katika wingu, maadui zao wakiwa wanawatazama.