7 Wakati miaka 1,000 itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka gerezani mwake.
8 Basi, atatoka nje, ataanza kuyapotosha mataifa yote yaliyotawanyika kila mahali duniani, yaani Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya pamoja kwa ajili ya vita; nao watakuwa wengi kama mchanga wa pwani.
9 Walipita katika nchi yote, wakaizunguka kambi ya watakatifu na mji wa Mungu aupendao. Lakini moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawaangamiza.
10 Naye Ibilisi aliyekuwa anawapotosha, akatupwa ndani ya ziwa linalowaka madini ya kiberiti, walimo yule mnyama na yule nabii wa uongo, nao watateswa mchana na usiku, milele na milele.
11 Kisha, nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe, na yule aketiye juu yake. Dunia na mbingu vikatoweka mbele ya macho yake, na havikuonekana tena.
12 Kisha nikawaona watu wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa. Halafu kitabu kingine, yaani kitabu cha uhai, kikafunguliwa pia. Wafu wakahukumiwa kadiri ya matendo yao, kama ilivyoandikwa ndani ya vitabu hivyo.
13 Bahari ikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yake; Kifo na Kuzimu vikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yao. Kila mmoja akahukumiwa kufuatana na matendo yake.