6 Yesu akawaambia, “Tupeni wavu upande wa kulia wa mashua nanyi mtapata samaki.” Basi, wakatupa wavu lakini sasa hawakuweza kuuvuta tena kwa wingi wa samaki.
7 Hapo yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi lake (maana hakuwa amelivaa), akarukia majini.
8 Lakini wale wanafunzi wengine walikuja pwani kwa mashua huku wanauvuta wavu uliojaa samaki; hawakuwa mbali na nchi kavu, ila walikuwa yapata mita mia kutoka ukingoni.
9 Walipofika nchi kavu waliona moto wa makaa umewashwa na juu yake pamewekwa samaki na mkate.
10 Yesu akawaambia, “Leteni hapa baadhi ya samaki mliovua.”
11 Basi, Simoni Petro akapanda mashuani, akavuta hadi nchi kavu ule wavu uliokuwa umejaa samaki wakubwa 153. Na ingawa walikuwa wengi hivyo, wavu haukukatika.
12 Yesu akawaambia, “Njoni mkafungue kinywa.” Hakuna hata mmoja wao aliyethubutu kumwuliza: “Wewe ni nani?” maana walijua alikuwa Bwana.