1 Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo na ndugu yake Yakobo, nawaandikia nyinyi mlioitwa na Mungu na ambao mnapendwa naye Mungu Baba, na kuwekwa salama kwa ajili ya Yesu Kristo.
2 Nawatakieni huruma, amani na upendo kwa wingi.
3 Ndugu wapenzi, nilikuwa na mpango wa kuwaandikieni juu ya ule wokovu tunaoshiriki sote, lakini nimeona lazima ya kuwaandikieni nikiwahimizeni mwendelee na juhudi kwa ajili ya imani ambayo Mungu amewajalia watu wake mara moja tu kwa wakati wote.
4 Maana watu wasiomcha Mungu wamepata kujiingiza kwa siri miongoni mwetu, watu ambao, kwa faida ya maisha yao mabaya, wanaupotosha ujumbe wa neema ya Mungu wetu na kumkana Yesu Kristo aliye peke yake Kiongozi na Bwana wetu. Lakini, Maandiko Matakatifu yalikwisha bashiri tangu zamani hukumu inayowangojea watu hao.
5 Sasa nataka kuwakumbusheni mambo fulani, ingawaje haya mlikwisha fahamishwa kikamilifu mara moja: Kumbukeni jinsi Bwana alivyowaokoa watu wa Israeli na kuwatoa katika nchi ya Misri, lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini.
6 Na, malaika ambao hawakuridhika na cheo chao, wakayaacha makao yao ya asili, Mungu amewafunga gizani kwa minyororo ya milele wahukumiwe siku ile kuu.
7 Kumbukeni pia Sodoma na Gomora, na miji ya kandokando yake; wenyeji wake walifanya kama wale malaika; walifanya uzinzi na mambo yaliyo kinyume cha maumbile, wakapewa hukumu ya moto wa milele, iwe onyo kwa watu wote.
8 Hivyo ndivyo pia walivyo watu hawa. Ndoto zao huwaongoza katika kuichafua miili yao wenyewe, kuyadharau mamlaka ya Mungu na kuvitukana viumbe vitukufu vya huko juu.
9 Hata Mikaeli, malaika mkuu, hakufanya hivyo. Katika ule ubishi kati yake na Ibilisi juu ya mwili wa Mose, Mikaeli hakuthubutu kumhukumu Ibilisi kwa matusi, ila alisema: “Bwana mwenyewe na akukaripie.”
10 Lakini watu hawa hutukana chochote wasichokielewa; wataangamizwa kwa mambo yaleyale wanayoyajua kwa silika kama wajuavyo wanyama wasio na akili.
11 Ole wao! Watu hao wamefuata mwenendo uleule wa Kaini. Kwa ajili ya fedha, wamejiingiza katika mkosi uleule wa Balaamu. Wameasi kama Kora alivyoasi na wameangamizwa kama yeye alivyoangamizwa.
12 Kwa makelele yao yasiyo na adabu, na kwa kujipendelea wao wenyewe, watu hao ni kama madoa machafu kwenye karamu mnazoshiriki kwa upendo. Wako kama mawingu yasiyo na mvua yanayopeperushwa na upepo. Wao ni kama miti iliyopukutika isiyozaa matunda, iliyokufa kabisa, iliyong'olewa.
13 Watu hao ni kama mawimbi makali ya bahari, na matendo yao ya aibu yanatoka kama povu. Wao ni kama nyota zinazotangatanga ambazo zimewekewa milele mahali pa giza kuu.
14 Naye Henoki, ambaye ni babu wa saba tangu Adamu, alibashiri hivi juu ya watu hao: “Sikilizeni! Bwana anakuja pamoja na maelfu ya malaika wake watakatifu
15 kuwahukumu watu wote, na kuwaadhibu wote wasiomcha Mungu kwa ajili ya matendo yao yote maovu waliyotenda bila kumjali Mungu, na kwa ajili ya maneno yote mabaya ambayo watu waovu walimkashifu nayo.”
16 Watu hawa hunung'unika daima, hulalamika, hufuata tamaa zao mbaya, hujigamba na kuwasifu watu wengine mno kwa faida yao wenyewe.
17 Lakini nyinyi wapenzi wangu, kumbukeni yale mliyoambiwa hapo awali na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo.
18 Waliwaambieni: “Siku za mwisho, watatokea watu watakaowadhihaki nyinyi, watu wafuatao tamaa zao mbaya.”
19 Hao ndio wanaosababisha mafarakano, watu wa fikira za kidunia, wasio na Roho wa Mungu.
20 Lakini nyinyi, wapenzi wangu, jijengeni wenyewe juu ya imani yenu takatifu kabisa. Salini kwa nguvu ya Roho Mtakatifu,
21 na kudumu katika upendo wa Mungu, mkimngojea Bwana wetu Yesu Kristo ambaye, kwa huruma yake, atawajalieni uhai wa milele.
22 Muwe na huruma kwa watu walio na mashaka;
23 waokoeni kwa kuwanyakua kutoka motoni. Lakini kwa wengine muwe na huruma pamoja na tahadhari, mkichukia hata mavazi yao yenye madoa ya tamaa zao mbaya.
24 Kwake yeye awezaye kuwalinda msije mkaanguka, na kuwaleta nyinyi bila hatia mpaka mbele ya utukufu wake,
25 kwake yeye aliye peke yake Mungu, Mkombozi wetu, uwe utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kwa njia ya Kristo Bwana wetu, tangu zama zote, sasa na hata milele! Amina.