4 Baadaye Daudi na Waisraeli wote walikwenda Yerusalemu uliojulikana kama Yebusi, na ambao wenyeji wake walikuwa Wayebusi.
5 Wakazi wa Yebusi walimwambia Daudi, “Hutaingia katika mji huu.” Hata hivyo, Daudi aliiteka ngome ya Siyoni, yaani mji wa Daudi.
6 Ndipo Daudi akasema, “Mtu atakayetangulia kuwapiga Wayebusi, atakuwa mkuu na kamanda jeshini.” Basi Yoabu, mwana wa Seruya, akawa wa kwanza kuwashambulia, hivyo akawa mkuu.
7 Daudi alikaa katika ngome hiyo, na kwa hiyo, mji huo ukaitwa “Mji wa Daudi.”
8 Aliujenga mji huo, akianzia Milo, na kuuzunguka wote, na Yoabu akautengeneza mji huo upya.
9 Naye Daudi akazidi kuwa mkuu kwa sababu Mwenyezi-Mungu wa majeshi alikuwa pamoja naye.
10 Hii ndiyo orodha ya wakuu wa mashujaa wa Daudi, ambao pamoja na watu wengine wote wa Israeli, walimuunga mkono kwa pamoja ili awe mfalme, sawa na neno la Mwenyezi-Mungu alilotoa juu ya Waisraeli.