7 Daudi alikaa katika ngome hiyo, na kwa hiyo, mji huo ukaitwa “Mji wa Daudi.”
8 Aliujenga mji huo, akianzia Milo, na kuuzunguka wote, na Yoabu akautengeneza mji huo upya.
9 Naye Daudi akazidi kuwa mkuu kwa sababu Mwenyezi-Mungu wa majeshi alikuwa pamoja naye.
10 Hii ndiyo orodha ya wakuu wa mashujaa wa Daudi, ambao pamoja na watu wengine wote wa Israeli, walimuunga mkono kwa pamoja ili awe mfalme, sawa na neno la Mwenyezi-Mungu alilotoa juu ya Waisraeli.
11 Ifuatayo ni orodha ya mashujaa hao wa Daudi: Yashobeamu, Mhakmoni, aliyekuwa kiongozi wa “Wale thelathini.” Yeye alipigana kwa mkuki wake akaua watu 300 kwa mara moja vitani.
12 Halafu aliyefuata miongoni mwa wale mashujaa watatu alikuwa Eleazari mwana wa Dodo, Mwahohi.
13 Siku moja Eleazari alikuwa pamoja na Daudi huko Pas-damimu, wakati Wafilisti walipokusanyika kupigana vita. Huko kulikuwa na shamba lenye shayiri tele, nao Waisraeli walikuwa wamewakimbia Wafilisti.