5 Hivyo, Daudi aliwakusanya Waisraeli wote nchini; toka kijito cha Shihori kilichoko Misri, hadi maingilio ya Hamathi ili kulileta sanduku la Mungu toka Kiriath-yearimu.
6 Daudi, akiandamana na Waisraeli wote, akaenda hadi mjini Baala, yaani Kiriath-yearimu, nchini Yudea, ili kulichukua toka huko sanduku la Mungu linaloitwa kwa jina lake Mwenyezi-Mungu akaaye kwenye kiti chake cha enzi juu ya viumbe vyenye mabawa.
7 Basi, wakalichukua sanduku la Mungu kutoka katika nyumba ya Abinadabu kwa gari jipya. Uza na Ahio waliliendesha gari hilo.
8 Daudi na Waisraeli wote wakawa wanacheza kwa nguvu zao zote, mbele ya Mungu. Waliimba huku wanapiga ala za muziki zilizotengenezwa kwa mvinje: Vinubi, vinanda, matari, matoazi na tarumbeta.
9 Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Kidoni, Uza aliunyosha mkono wake kulishikilia sanduku la agano kwa sababu ng'ombe walijikwaa.
10 Mara Mwenyezi-Mungu akamkasirikia Uza kwa kulishika sanduku, akamuua. Uza akafa papo hapo mbele ya Mungu.
11 Daudi alikasirika kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimuua Uza akiwa na hasira. Kwa sababu hiyo, mahali hapo huitwa Peres-uza hadi leo.