1 Wakati mfalme Daudi alipokuwa akikaa katika ikulu, siku moja alimwita nabii Nathani, na kumwambia, “Hebu tazama, mimi ninakaa kwenye nyumba nzuri iliyojengwa kwa mwerezi, lakini sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu linakaa hemani.”
2 Nathani akamwambia Daudi, “Fanya chochote unachofikiria moyoni mwako, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.”
3 Lakini usiku uleule, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Nathani, kusema,
4 “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Wewe hutanijengea nyumba ya kukaa.
5 Tangu wakati ule nilipowaongoza watu wa Israeli kutoka Misri mpaka hivi leo, sijaishi kwenye nyumba. Nimekuwa nikihama toka hema hadi hema, na toka makao hadi makao mengine.
6 Je, kila mahali ambako nimekwenda na Waisraeli, nimepata kumwuliza mwamuzi wao yeyote niliyemwamuru awachunge watu wangu, “Kwa nini hukunijengea nyumba ya mierezi?” ’