12 Yeye ndiye atakayenijengea nyumba; nami nitahakikisha kwamba ufalme wake unadumu milele.
13 Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; lakini sitamwondolea fadhili zangu kama vile nilivyomwondolea Shauli aliyekutangulia.
14 Bali nitamwimarisha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele, na kiti chake cha enzi kitakuwa imara daima.’”
15 Nathani alimwelezea Daudi mambo yote haya kulingana na maono yote.
16 Kisha mfalme Daudi akaingia ndani ya hema na kuketi mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu akaomba, “Mimi ni nani, ee Mwenyezi-Mungu, na nyumba yangu ni nini hata unitukuze hivi?
17 Isitoshe, umenifanyia mengine zaidi: Umenitolea ahadi juu ya vizazi vyangu vijavyo ee Mwenyezi-Mungu!
18 Nikuambie nini zaidi, mimi Daudi mtumishi wako, kwa kunitukuza hivyo? Wewe unanijua mimi mtumishi wako.