6 Je, kila mahali ambako nimekwenda na Waisraeli, nimepata kumwuliza mwamuzi wao yeyote niliyemwamuru awachunge watu wangu, “Kwa nini hukunijengea nyumba ya mierezi?” ’
7 Kwa hiyo basi, mwambie mtumishi wangu Daudi: ‘Mwenyezi-Mungu wa majeshi anasema hivi: Nilikutoa malishoni ulipokuwa unawachunga kondoo, ili uwe mkuu wa watu wangu Israeli.
8 Tangu wakati huo nimekuwa pamoja nawe kokote ulikokwenda na nimewaangamiza maadui zako wote mbele yako. Nitakufanya kuwa maarufu kama wakuu wengine wa dunia.
9 Nami nitawachagulia watu wangu wa Israeli mahali pa kuishi niwapandikize, ili waishi mahali pao wenyewe, wasisumbuliwe tena. Nao watu wakatili wanaotumia nguvu hawatawatesa tena kama hapo awali,
10 tangu wakati nilipowateua waamuzi juu ya watu wangu Israeli; mimi nitawashinda maadui zako wote. Zaidi ya yote, mimi Mwenyezi-Mungu nakutangazia kuwa nitakujengea nyumba.
11 Siku zako zitakapotimia za kujiunga na babu zako, nitamfanya mmoja wa watoto wako, wewe mwenyewe awe mfalme; nami nitauimarisha ufalme wake.
12 Yeye ndiye atakayenijengea nyumba; nami nitahakikisha kwamba ufalme wake unadumu milele.