12 Mwenyezi-Mungu akupe busara na akili ili atakapokupa uongozi juu ya Israeli, uzishike sheria zake Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.
13 Ukiwa mwangalifu, na ukizitii amri ambazo Mwenyezi-Mungu alimwagiza Mose juu ya Israeli, utastawi. Jipe moyo, uwe imara. Usiogope wala usifadhaike.
14 Kwa juhudi kubwa, nimeiwekea akiba nyumba ya Mwenyezi-Mungu, talanta 100,000 za dhahabu, talanta 1,000,000 za fedha na idadi isiyopimika ya shaba na chuma, kwani ni nyingi sana. Nimeandaa mbao na mawe tayari. Lakini huna budi kuongezea.
15 Unao wafanyakazi wengi: Kuna wachonga mawe, waashi, maseremala na mafundi wa kila aina wenye ujuzi mwingi;
16 wa kufua dhahabu, fedha, shaba na chuma. Haya! Anza kazi! Mwenyezi-Mungu na awe pamoja nawe!”
17 Zaidi ya hayo, Daudi aliwaamuru viongozi wote wa Waisraeli wamsaidie Solomoni mwanawe, akisema,
18 “Je, Mwenyezi-Mungu Mungu wenu hayuko pamoja nanyi? Je, hajawapa amani katika pande zote? Yeye aliwatia wakazi wa nchi hii mikononi mwangu na sasa wako chini ya Mwenyezi-Mungu na watu wake.