8 Lakini Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Wewe umemwaga damu nyingi kwa kupigana vita vikubwa. Kwa sababu ya damu nyingi ambayo umemwaga mbele yangu hapa duniani, hutanijengea nyumba.
9 Hata hivyo, utapata mwana, ambaye atatawala kwa amani kwa sababu nitampa amani na maadui zake wote wa jirani. Jina lake litakuwa Solomoni, kwa maana katika siku za utawala wake, atailetea Israeli amani na utulivu.
10 Hivyo, yeye ndiye atakayenijengea nyumba. Atakuwa mwanangu nami nitakuwa baba yake, na wazawa wake wataitawala Israeli milele.’
11 Sasa mwanangu, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako na awe pamoja nawe ili ufaulu kumjengea nyumba kama alivyosema.
12 Mwenyezi-Mungu akupe busara na akili ili atakapokupa uongozi juu ya Israeli, uzishike sheria zake Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.
13 Ukiwa mwangalifu, na ukizitii amri ambazo Mwenyezi-Mungu alimwagiza Mose juu ya Israeli, utastawi. Jipe moyo, uwe imara. Usiogope wala usifadhaike.
14 Kwa juhudi kubwa, nimeiwekea akiba nyumba ya Mwenyezi-Mungu, talanta 100,000 za dhahabu, talanta 1,000,000 za fedha na idadi isiyopimika ya shaba na chuma, kwani ni nyingi sana. Nimeandaa mbao na mawe tayari. Lakini huna budi kuongezea.