1 Samueli akawaambia Waisraeli wote, “Yote mliyoniambia, nimeyasikiliza. Nimemtawaza mfalme juu yenu.
2 Sasa, mnaye mfalme wa kuwaongoza. Kwa upande wangu, mimi ni mzee mwenye mvi, na watoto wangu wa kiume wako pamoja nanyi. Nimekuwa kiongozi wenu tangu nilipokuwa kijana mpaka sasa.
3 Niko hapa, na kama nimefanya tendo lolote lile baya, basi, toeni ushahidi mbele ya Mwenyezi-Mungu na mbele ya mfalme wake mteule. Je, nimepora fahali au punda wa mtu yeyote? Je, nimempunja mtu yeyote? Je, nimemkandamiza mtu yeyote? Je, nimepokea rushwa kwa mtu yeyote ili kupotosha haki? Nami nitamrudishia chochote kile.”
4 Watu wakamjibu, “Kamwe hujatudanganya, hujatukandamiza, wala hujachukua kitu chochote kwa mtu.”