26 Mtoto Samueli aliendelea kukua, akazidi kupendwa na Mwenyezi-Mungu na watu.
27 Siku moja, mtu wa Mungu alimwendea Eli, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Nilijijulisha kwa jamaa ya Aroni, wazee wako, walipokuwa watumwa wa Farao nchini Misri.
28 Kati ya makabila yote ya Israeli nilimchagua Aroni na jamaa yake kuwa makuhani wangu, wanitumikie madhabahuni, wafukize ubani na kuvaa kizibao mbele yangu. Nikaipatia jamaa ya mzee wako tambiko zangu ambazo Waisraeli walinitolea kwa moto.
29 Kwa nini basi, umezionea wivu tambiko na sadaka nilizowaamuru watu waniletee? Wewe umewastahi watoto wako kuliko mimi kwa kujinenepesha nyinyi wenyewe kwa kula sehemu nzurinzuri za sadaka ambazo watu wangu wa Israeli hunitolea!’
30 Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anatamka hivi, ‘Niliahidi kwamba jamaa yako na jamaa ya wazee wako mtakuja mbele yangu kunitumikia milele;’ lakini sasa Mwenyezi-Mungu anakutangazia hivi, ‘Jambo hilo liwe mbali nami.’ Nitawaheshimu wale wanaoniheshimu, na wale wanaonidharau, nitawadharau.
31 Angalia siku zaja ambapo nitawaua vijana wote wa kiume katika jamaa yako na katika ukoo wako, hata hakutakuwa na mwanamume yeyote atakayeishi awe mzee.
32 Utakuwa na wasiwasi na utawaonea wenzio kijicho kwa zile baraka zote ambazo nitawapa watu wengine wa Israeli, lakini hakuna mtu katika jamaa yako atakayeishi na kuwa mzee.