10 Siku hiyo, Daudi alimkimbia Shauli, akaenda kwa mfalme Akishi wa Gathi.
11 Watumishi wa mfalme wakamwambia Akishi, “Huyu si Daudi, mfalme wa nchi ya Israeli? Je, si huyu ambaye walikuwa wakiimbiana juu yake katika ngoma, wakisema, ‘Shauli ameua maelfu yake na Daudi ameua makumi elfu yake?’”
12 Maneno hayo Daudi hakuweza kuyasahau, akaanza kumwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi.
13 Hivyo, akabadilisha tabia yake, akijifanya mwendawazimu, akawa anakwaruzakwaruza kwenye malango ya mji, na mate yake akayaacha yatiririke kwenye ndevu zake.
14 Akishi akawaambia watumishi wake, “Mnajua kuwa mtu huyu ni mwendawazimu; kwa nini mmemleta kwangu?
15 Je, nawahitaji wendawazimu zaidi? Kwa nini mnaniletea mwendawazimu aje kunisumbua na vitendo vya wendawazimu? Je, mtu huyu ataingia nyumbani kwangu?”